Baba Riz Awauza Chadema

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa kitendo cha Baba Riz kusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011, kimekiuka makubaliano yao, hivyo kimeamua kususia mchakato mzima wa kuratibu maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia sheria hiyo.Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuonyesha kutoridhishwa na namna kiongozi huyo wa nchi, alivyowachezea akili.

“Kitendo cha Rais Kikwete kuusaini muswada huo bila ya kuupitia ni kinyume na makubaliano, jambo ambalo linatufanya tususie mchakato mzima wa kuuratibu maoni ya kwa ajili ya Katiba Mpya kupitia sheria ailiyoisaini,”alisema Mnyika na kuendelea:

“Tumeamua kujitoa kwenye mchakato mzima wa kuratibu Marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Katiba kutokana na Rais kukiuka makubaliano yetu Ikulu yaliyomtaka aupitie kwanza kabla ya kuusaini.”  Mnyika aliendelea kueleza kuwa Chadema iliwasilisha waraka wa mapendekezo sita kwa Rais ikiwa ni pamoja na kumtaka asiusaini muswada huo kutokana na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo kwenye mchakato wa ukusanyaji wa maoni.

Alisema mapendekezo mengine ni uundaji wa tume huru, upatikanaji wa uwakilishi kutoka pande zote mbili za Muungano; Zanzibar na Bara ili kutoa fursa ya kupata maoni yao katika marekebisho hayo.  “Suala la tatu ni uundaji wa Bunge la Katiba na kupunguza mamlaka ya Rais na jambo la nne ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano pamoja na mfumo mzima wa uwakilishi wa pamoja katika muundo wa Bunge la Katiba.”

Mnyika alisema kutokana na hali hiyo iliyojitokeza ya Rais kutowasikiliza, watawasilisha waraka huo waliompa, kwa wananchi ili nao wausome na kutoa maoni yao.

Alisema katika kutekeleza mkakati huo, hawatafanya maandamano yeyote, isipokuwa watatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya Katiba wanayopaswa kuwa nayo.

“Nia yetu ni mzuri, lengo ni kuboresha upatikanaji wa Katiba iwe bora na itakayoweza kutoa nafasi ya ushiriki wa pande zote. Lakini kinachofanyika sasa ni kinyume. Tumeamua kuwarudishia wananchi wenyewe ili waweze kuamua kama tumekosea au la,”alieleza.  Tamko hilo la Chadema limekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kutia saini muswada huo hivyo kuufanya kuwa sheria.
Baba Riz alitia saini muswada huo ikiwa ni siku moja baada ya yeye na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kukubaliana kwamba ipo haja ya kuendelea kuuboresha muswada ili ukidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa.  Pia, walikubaliana yawepo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

CUF nao wakubaliwa kukutana na Baba Riz
Katika hatua nyingine, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili kujadili Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 2011, iliyotiwa saini juzi na mkuu huyo wa nchi.  Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa baada ya kupata ombi hilo, Baba riz alikubali kukutana nao.

“Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka CUF kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba Riz,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:  ” Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano huo yafanyike mara moja.”

9 comments - What do you think?
Posted by admin - December 1, 2011 at 5:26 am

Categories: Habari   Tags:

Baba Riz,Chadema wakubaliana kuboresha muswada

Baba Riz na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wamekubaliana kwamba ipo haja ya kuendelea kuuboresha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ili ukidhi mahitaji ya kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.Pia, wamekubaliana yawepo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku mbili baina ya pande hizo mbili kuhusu muswada huo.

Katika kikao cha jana Mbowe aliongozana na wajumbe wa kamati hiyo Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Said Arfi na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu na John Mrema.

Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa ambaye ni mjumbe hakuwapo katika kikao cha juzi na cha jana na taarifa zilizopatikana baadaye na kuthibitishwa na yeye mwenyewe ni kwamba alikuwa safarini kwenda kuhudhuria kesi yake mahakamani Arusha jana.

Kabrasha lililokabidhiwa na ujumbe wa Chadema kwa Rais Kikwete lilikuwa lina waraka uliotoa mapendekezo mbalimbali ya kurekebisha muswada huo huku wakitaka sheria iweke wazi kwamba Rais hana mamlaka yoyote juu ya Bunge Maalum la Katiba zaidi ya mamlaka ya kuliitisha kwa mara ya kwanza na kwamba mamlaka ya Bunge hilo yataisha mara baada ya kupitishwa kwa Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba.

3 comments - What do you think?
Posted by admin - November 29, 2011 at 4:13 am

Categories: Habari   Tags:

UDSM yawasimamisha 22, 50 wapandishwa kizimbani

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wanafunzi 22, ambao wanadhaniwa kuwa vinara wa mgomo uliofanyika Novemba 11.

Wakati huohuo ,wanafunzi 50 wa sehemu ya mlimani jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali.

Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya aliwataja washtakiwa hao kuwa, ni Wambapa Elias, Evanis Elias, Baraka Monas, Hellen Moshi,  Alphonce Lusako, Matrona Babu, Rolanda Wilfred, Godfrey Deogratius, Moris Denis, Evon Lujuko Mathias, Ndimbo Jabir, Evarist Wilson, Cornel Rwaga, Mushi Michael, Mlazi Kumbuka, Baraka John, Ayoub Oscar, Maduhu Japhet, Salehe Twalibu.

Wengine ni Ganus Ibrahim, Alaxander Wasanga, Adorinoriz Alphonce, Rehema Munuo , Glory Masawe, Happy Amulike, Elisia Mpangala, Frida Timoth, Stellah Msofe, Charles Mwakajile, Said John, Reyson Masasi, Betwel Martin, Peter Lutufyo, Mmasy Stephen na Mtenga Honoli. Wamo pia Modekae Francis, Anthony Mganyizi, Wilbroad Eanes, Paulo Muna, Raphael Jonathan, Lugemila Venance, Domina Fulgence, Rehema Juma, Luciana Ismaikl, Lina Happygod, Asha Twaha, Jenifa Kameta, Francisca Mduma na Neema Majaliwa.

 

8 comments - What do you think?
Posted by admin - November 15, 2011 at 3:20 am

Categories: Uncategorized   Tags:

Mbowe apandishwa kizimbani na wanafunzi 46 UDSM wakamatwa

MWENYEKITI wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, amepandishwa kizimbani katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa kutii amri ya polisi

Na vile vile wanafunzi 46 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanashikiliwa na polisi baada ya kuandamana bila kibali kushinikiza Serikali kuwapa mikopo wenzao 1,000 waliokosa. Kabla ya kukamatwa,  Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kililazimika kutumia mabomu ya machozi na vipigo dhidi ya wanafunzi hao waliokuwa wakiandamana kuelekea Ubungo.

Maandamano hayo yalianza saa 3:30 asubuhi kwa wanafunzi hao kupita madarasani kuwalazimisha wenzao kujiunga nao, huku waliopinga wakipigwa. Hatua hiyo, ilisababisha wengi wa wanafunzi hao kulikimbia huku na kule kuwakwepa waandamanaji hao waliokuwa na hasira, wakitumia fimbo ndefu kuwaadhibu walioktaa kujiunga nao. Baadaye safari ya kuelekea Ubungo ilianza lengo likiwa kufikisha ujumbe wao nje ya chuo hicho.

Baada ya kufika lango kuu la kuingilia chuoni hapo karibu na Ubungo, kulikuwa na magari ya FFU aina ya Landarover 110 na malori mawili yenye maji ya kuwasha.

Waandamanaji hao hata baada ya kuyaona magari hayo hawakusita, waliendelea kusonga mbele. Walipofika langoni hapo mabomu ya machozi yalianza kurushwa na walianza kukimbia na wengine wakipigwa na kukamatwa. Katika muda usiozidi dakika 10, zoezi lilikuwa limemalizika, magari yalikuwa yamejaa wanafunzi waliokamatwa huku wengine wakikimbia.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Pamillius Wambura, alithibitisha kushikiliwa wanafunzi hao Kituo cha Oysterbay. Wambura alisema wanafunzi hao wanatuhumiwa kuandamana bila kibali.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe

31 comments - What do you think?
Posted by admin - November 11, 2011 at 10:23 pm

Categories: Habari   Tags:

Wanajeshi Wa DRC Wenye Silaha Wavamia Tanzagiza

KIKUNDI cha askari wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo Congo DRC wakiwa na silaha nzito za kivita wametia nanga katika Bandari ya Kigoma kwa madai ya kuwasaka waasi wanaopigana na Serikali ya nchi hiyo waliokimbilia hapa kutafuta matibabu.

Askari hao waliowasili hapa juzi jioni wakiwa katika boti ya kijeshi, walipenya bila kikwazo chochote na kuegesha jirani na boti ya polisi na ndipo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipopewa taarifa ya uvamizi huo na mara moja liliwasili katika eneo hilo na kuwaweka wanajeshi hao chini ya ulinzi.

Akizungumzia na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kikosi cha 24 KJ, Luteni Kanali Emmanuel Mcheri alisema wanajeshi hao wa DRC wapatao 20 waliingia Kigoma kinyume cha utaratibu jambo ambalo ni kosa kwa vile kitendo hicho kinaweza kusababisha vita baina ya nchi hizi mbili.

Alisema askari hao wa DRC walikuwa wakiongozwa na Luteni Kanali Mohamed Mustafa wa Kikosi cha Askari wa Miguu cha 42 chenye makazi yake Mashariki ya DRC ambaye alisema walikuja kufanya operesheni maalumu kuwasaka waasi wa nchi hiyo waliokimbilia Kigoma kutafuta huduma ya matibabu.

“Hawa Askari 20 kutoka DRC wamevuka mpaka kinyume cha sheria na kuvamia mkoani kwetu. Wameingia hadi kwenye bandari yetu ya Kigoma. Askari wetu wamewapekua na kuwanyang’anya silaha zote walizokuwa. Tunawashikilia hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine,” alisema Luteni Kanali Mcheri.
Askari hao walipelekwa katika Gereza la Bangwe.

Alitaja aina ya silaha walizokuja nazo ni bunduki 17 aina ya SMG, bunduki moja aina ya LMG, pistol moja ya, RPG moja, bomu moja la kutupwa kwa mkono na makombora matatu ya milimita 12 na milimita 16 yenye uwezo wa kutungua ndege.

“Lakini pia wamekuja na shehena kubwa ya risasi na tulipowapekua tumekamata magazini 32 za SMG zikiwa na jumla ya risasi 960, risasi tano za pistol, risasi za LMG zilikuwapo 360, lakini walikuja na boksi lililojaa risasi. Kwa kweli wamekiuka taratibu za kuingia nchini hata kama wanadai walikuwa katika operesheni yao kuwasaka waasi wanaopigana na Serikali yao” alisema.

Kuhusu kuingia bila ya kupata kikwazo chochote hadi bandarini, Luteni Kanali Mcheri alisema licha ya tukio hilo, askari wa JWTZ wapo imara kukabiliana na tishio lolote la uvamizi kutoka mahali popote.

“Mpaka wa mkoa wetu na nchi jirani ni mkubwa sana hivyo suala la ulinzi wa mipaka wakati mwingine linakuwa gumu sana, lakini bado nawahakikishia kwamba vijana wetu wapo imara kwa lolote na wala jambo hili lisiwatie hofu hata kidogo,” alisema.
Katika kikosi hicho cha askari wa DRC walikuwapo maofisa wanane wa jeshi, askari wa kawaida kumi na mmoja na raia mmoja anayedaiwa kuwa ni fundi wa boti hiyo la kijeshi.

Habari za ndani zinasema kuwa kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma ilikutana kwa dharura katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hata hivyo, haikufahamika mara moja kilichojitokeza katika kikao hicho.

Mnamo Novemba 3, mwaka huu, kundi la watu tisa waliodaiwa kuwa ni waasi wa DRC wakiwa na majeraha yanayoaminika kuwa ni kutokana na kushambuliwa kwa risasi, waliingia mkoani Kigoma kupitia Kijiji cha Mtanga ambako kuna Kituo kidogo cha JWTZ na hivyo kujikuta wakitiwa mbaroni kirahisi.

Baada ya kukamatwa, waasi hao walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kupata matibabu kutokana na majeraha hayo. Inadaiwa kuwa mmoja wao ameshafariki dunia.

20 comments - What do you think?
Posted by admin - November 8, 2011 at 4:08 am

Categories: Habari   Tags:

Yarabi Toba! Mkatae Huyo Shoga – Baba Riz

TANZANIA imesema ipo tayari kukosa  misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza  na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe,  alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.

“ Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga  upuuzi huo ambapo  Januari mwaka huu,  ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa  nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi  anayotoka.

“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua  kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Baba Riz kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!”

Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.

Alisema alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu.  “ Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.

Alieleza kuwa  tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama  Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo

Akisisitiza msimamo huo wa serikali, Membe,  alisema  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti,  yaani mume na mke.  “ Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.

Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano  Perth .

Hoja ya  kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.

35 comments - What do you think?
Posted by admin - November 4, 2011 at 4:28 am

Categories: Habari   Tags:

Vurugu Arusha na Mwanza Risasi, Mabomu Vyarindima

VURUGU kubwa zimetokea jana katika majiji ya Arusha na Mwanza kiasi cha kuwalazimu polisi kutumia mabiomu ya machozi na baadhi ya watu kutiwa nguvuni.Jana asubuhi jijini Arusha, watumishi wa daladala zinazojulikana huko kama vifodi, waliitisha mgomo kulaani kile walichokiita unyanyasaji wa polisi hatua iliyowalazimu askari hao kuingilia kati na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 30.

Mgomo huo ulianza majira ya saa mbili asubuhi na kudumu hadi saa 5:00 asubuhi.

Pia polisi na askari wa Magereza walikuwa na kibarua kizito kuwadhibiti wafuasi wa Chadema kwenda katika Gereza la Kisongo kumwona Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Polisi waliweka ulinzi mkali wakiwazuia na kuwahoji watu wote waliokuwa wakielekea njia ya Kisongo liliko Gereza hilo Kuu la Mkoa wa Arusha ambako Lema yuko mahabusu.

Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wanataka kwenda kumwona mbunge huyo katika utaratibu wa kawaida wa kuwaona wafungwa na mahabusu katika gereza hilo siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.

Baadhi ya wananchi waliofanikiwa kupenya kupitia njia za vichochoroni na kufika gerezani hapo, walikumbana na kizingiti kingine cha askari Magereza ambao waliwazuia kumwona mbunge huyo kwa madai idadi ya watu inayotakiwa kumwona ilishatimia.

19 comments - What do you think?
Posted by admin - November 3, 2011 at 9:22 am

Categories: Uncategorized   Tags:

Shujaa Lema Kajitoa Sadaka – Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema kitendo kilichofanywa na mbunge wa Arusha Godbless Lema ni cha kishujaa na kinapaswa kuungwa mkono na wafuasi wa Chadema kote nchini.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC jana jioni kuhusu kitendo cha Lema kukataa dhamana, Mbowe amesema matendo ya jeshi la polisi dhidi ya wafuasi wa chadema Arusha yamevuka mipaka na hayavumiliki tena.

Mbowe amesema mbunge Lema ameamua kujitoa sadaka kwa ajili ya wananchi na wafuasi wote wa chadema wanaoteseka kwa ajili ya kutafuta haki.

Mbowe amewataka wanachadema wote kutembea vifua mbele kwa ajili ya shujaa Lema.

9 comments - What do you think?
Posted by admin - November 1, 2011 at 6:32 am

Categories: Habari   Tags:

David Cameron Amtaka Baba Riz Atambue Haki za Mashoga

PERTH, Australia  UINGEREZA imetoa shinikizo la kutambua haki za mashoga kwa nchi zinazoendelea na kutishia kusitisha misaada yake kwa nchi zinazokiuka agizo hilo.  Waziri Mkuu David Cameron amesema Uingereza ina mpango ya kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria zake hazitambui ndoa za jinsia moja na mashoga.

“Nimeshawajulisha baadhi ya wakuu wa nchi kuhusu suala hilo kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Perth, Australia,” alisema Cameron kupitia BBC.Nchi 41 kati ya nchi 54 wanachama wa Jumuiya ya Madola, zina sheria zinazopinga ndoa za jinsia moja.

Suala la haki za binadamu ni moja ya agenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano huo ambao rais Kikwete pia alihudhuria.  Cameron alisema: “Tunasema hii ni moja ya vitu vinavyoongoza sera yetu ya misaada kwa mataifa mbalimbali na tayari tumeanza kuitekeleza katika maeneo kadhaa,” alisema.

Aliendelea: “Nchi zote zinazopata misaada kutoka kwetu (Uingereza), zinapaswa kukubaliana kikamilifu na sera hii ya haki za binadamu,” alisema.  Cameron alisema ameshazungumza na nchi mbalimbali za Afrika kuhusu suala hilo na utekelezaji wake utafanywa na Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo, William Hague.

Kukomesha vizuizi vya ndoa ya jinsia moja, ilikuwa moja ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya ndani ya matarajio ya baadaye  ya Jumuiya za Madola.  Katika mkakati huo, Uingereza imetishia kusitisha sehemu ya misaada ya bajeti kuu kwa nchi zisizokubaliana na msimamo huo lakini imeahidi kwamba haitaondoa bajeti yote.

33 comments - What do you think?
Posted by admin - November 1, 2011 at 3:11 am

Categories: Habari   Tags:

Zitto Apelekwa India, Aomba Kuombewa

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda juzi alikuwa miongoni mwa viongozi mbalimbali wa kitaifa waliofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kumjulia hali, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe muda mfupi kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema, anakuwa kiongozi wa nne kupelekwa India kwa matibabu katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, akitanguliwa na mawaziri wawili na naibu waziri mmoja. Hao ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Mbali ya Pinda, viongozi wengine waliofika kumjulia hali mbunge huyo ambaye alikuwa amelazwa katika chumba za uangalizi maalumu (ICU) ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed.

Katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, viongozi kadhaa wa Serikali wakiwamo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira walimjulia hali na kumtakia safari njema.

Zitto aliwataka Watanzania kuondoa hofu na badala yake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kushiriki katika Mkutano wa 10 wa Bunge.“Naendelea vyema, naomba Watanzania waelewe hivyo, waondoe wasiwasi na uvumi unaoenezwa,” alisema Zitto.

Alisema tangu aanze kupata matibabu Muhimbili, amemudu kula chakula kama kawaida na hali ya uchovu imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, alisema: “Ninakwenda India kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwani kichwa kinauma,” alisema.

Zitto aliondoka juzi mchana akiwa na kaka yake, Salum Kabwe na mmoja wa wauguzi wa Muhimbili ambaye jina lake halikufahamika mara moja.

30 comments - What do you think?
Posted by admin - October 29, 2011 at 8:12 am

Categories: Habari   Tags:

Next Page »